Swahili.Bible
Bible Society of Kenya
Bible Society of Kenya
Madaraka, Nairobi
PO Box 72983
Tel: 254 20602807
E-mail: info@biblesociety-kenya.org
1
Waisraeli Waonewa
1Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli ambao walikwenda Misri na Yakobo, kila mmoja akiwa pamoja na jamaa yake: 2Reubeni, Simeoni, Lawi na Yuda; 3Isakari, Zabuloni na Benyamini; 4Dani na Naftali, Gadi na Asheri. 5Wazao wote wa Yakobo walikuwa watu sabini; Yosefu alikuwa tayari yuko Misri.
6Basi Yosefu na kaka zake wote na kizazi kile chote walikufa, 7lakini Waisraeli walikuwa wamezaana na kuongezeka sana, idadi yao ikawa kubwa mno, kwa hiyo wakaijaza nchi.
8Kisha mfalme mpya ambaye hakufahamu habari za Yosefu akatawala Misri. 9Akawaambia watu wake, “Tazameni, Waisraeli wamekuwa wengi mno kwa idadi kutuliko sisi. 10Njooni, ni lazima tuwashughulikie kwa uangalifu, la sivyo watazidi kuwa wengi zaidi, na ikiwa patatokea vita, watajiunga na adui zetu kupigana dhidi yetu na kuondoka katika nchi hii.”
11Basi Wamisri wakaweka wasimamizi wa kuwasimamia na kuwatesa Waisraeli kwa kazi ngumu, nao wakajenga miji ya Pithomu na Ramesesi ya kuweka akiba ya Farao. 12Lakini walivyozidi kuteswa ndivyo walivyozidi kuongezeka na kuenea katika nchi; Wamisri wakawaogopa Waisraeli, 13kwa hiyo wakawatumikisha kwa ukatili. 14Wakafanya maisha ya Waisraeli kuwa machungu kwa kufanya kazi ngumu ya kutengeneza lami na kufyatua matofali, na kazi zote za mashambani; katika kazi zao zote ngumu, Wamisri waliwatumia Waisraeli kwa ukatili.
15Mfalme wa Misri akawaambia wakunga wa Kimisri waliowazalisha wanawake wa Kiebrania, ambao majina yao ni Shifra na Pua, 16“Mtakapowazalisha wanawake wa Kiebrania, chunguzeni wanapojifungua. Ikiwa ni mtoto wa kiume, muueni, lakini ikiwa ni msichana, mwacheni aishi.” 17Lakini hao wakunga walimcha Mungu na hawakufanya kile mfalme wa Misri alichowaambia kufanya, bali wakawaacha watoto wa kiume waishi. 18Ndipo mfalme wa Misri akawaita hao wakunga, akawauliza, “Kwa nini mmefanya hivi? Mbona mmeacha watoto wa kiume waishi?”
19Wakunga wakamjibu Farao, “Wanawake wa Kiebrania ni tofauti na wanawake wa Kimisri; wao wana nguvu, nao hujifungua watoto kabla wakunga hawajafika.”
20Kwa hiyo Mungu akawatendea mema wakunga hao. Waisraeli wakaongezeka na kuendelea kuwa wengi zaidi. 21Kwa vile hao wakunga walimcha Mungu, Mungu akawajalia kuwa na jamaa zao wenyewe.
22Kisha Farao akatoa agizo hili kwa watu wake wote: “Kila mtoto wa kiume atakayezaliwa kwa Waebrania lazima atupwe katika Mto Naili, bali kila mtoto wa kike aachwe aishi.”